Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Huku mvua ikiendelea kunyesha katika eneo la Pwani, familia zinazoishi mitaani zimeitaka serikali ya Kaunti ya Mombasa kuwatafutia makazi mbadala.

Wakazi hao ambao wameweka makao ya muda katika maneo mbalimbali ya umma, walisema kuwa wanahofia kuwa huenda mvua inayonyesha ikawasababishia maradhi yanayoletwa na baridi.

Kwenye mahojiano na mwandishi huyu siku ya Alhamisi katika eneo la posta ambapo wao hukusanyika kuomba msaada kutoka kwa wasamaria wema, wakazi hao walisema kuwa serikali ya kaunti imewasahau na kutoa wito kwa vyombo vya habari kuwasalisha masaibu yao kwa gavana wa Kaunti hiyo Hassan Joho.

Wakiongozwa na mama Salma Kombo, familia hizo zilisema kuwa zimekumbwa na matatizo mengi kwa sababu ya kuwa na watoto wadogo ambao wengi wako chini ya umri wa miaka miwili, ambao wanahitaji kupewa ulinzi na kulindwa kwa umakini mkubwa dhidi ya kuvamiwa na maradhi mbalimbali.

“Tulifurushwa na maafisa wa Kaunti ya Mombasa kutoka kwenye maeneo tuliyokuwa tukitekeleza biashara zetu mbalimbali. Hali hiyo ilichangia kuzorota kwa uchumi miongoni mwetu na kutusababisha kutegemea kuomba msaada kutoka kwa wapiti njia na mashirika mengine ya ufadhili wa kijamii,” alisema Kombo.

Familia hizo ambazo asilimia 95 hujumuisha kina mama na watoto zimeweka kambi katika maeneo ya Bauxton, Tononoka, uga wa kufanyia hadhara wa Makadara pamoja na eneo la Posta.