Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho pamoja na viongozi wengine waliongoza wananchi  wa kaunti hiyo katika zoezi la kuzoa takataka siku ya Jumamosi lililofanyika  katika mitaa ya Changamwe.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akiongea  baada ya zoezi hilo, Joho alisema kuwa wameanzisha kampeni ya kudhibiti takataka katika shule za kaunti hiyo.

Kampeni hiyo inalenga kuwafunza wanafunzi njia mbadala za kukusanya pamoja na kuhifadhi takataka ili kupunguza uharibifu wa mazingira pamoja na kuhakikisha afya bora.

“Tunataka kuwafunza watoto wetu jinsi ya kuweka mazingira safi kwa ajili ya afya kwao pamoja na jamii kwa ujumla,” alisema gavana.

Hatua hiyo imepokelewa vizuri na wakaazi hao ambao wengi walionekana kushirikiana vyema na viongozi katika zoezi hilo.

Eneo la Changamwe ni moja kati ya mitaa ya Mombasa inayoshuhudia idadi kubwa ya takataka zinazojaa katika sehemu ya kutupa, na wakaazi wamekuwa wakilalamikia serikali ya kaunti kuharakisha shughuli ya uzoaji wa taka hizo ili kuwaondolea athari ya kupata maradhi.

Hata hivyo, serikali ya kaunti imejitahidi kwa kununua magari ya kuzoa takakata yaliyosambazwa maeneo kadhaa kutekeleza kazi hiyo, japo wakaazi wanataka shughuli hiyo kuimarishwa zaidi kwani wamekuwa wakilalamika kwamba mara nyingi magari hayo hujaa lakini yakaa siku kadhaa kabla hayajaondolewa.