Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mbunge wa Nakuru mjini amesifiwa na viongozi tofauti waliohudhuria hafla ya kuwaelimisha wananchi kuhusu chama kipya cha JPK, mkutano ulioandaliwa katika afisi za chama cha TNA Milimani Nakuru.

Wakizungumza mmoja baada ya mwingine, wakazi hao walimpongeza mbunge wa Nakuru Mjini David Gikaria kwa kuwaunganisha wakazi wa Nakuru mjini ambao huwajumuisha makabila tofauti.

Aliyekuwa mwenyekiti wa chama cha URP tawi la Nakuru Joseph Kipkurui Bett amemtaja Gikaria kama kiongozi na mwanasiasa mwenye busara kwa kuleta pamoja jamii za tabaka mbalimbali, huku akiomba viongozi wengine kuiga mfano wake.

Mchamganuzi wa masuala ya kisiasa Daktari Abdi Noor alisema Gikaria ni mfano mwema kwa uongozi bora katika Kaunti ya Nakuru, huku akimsuta mwanasiasa Stanley Karanja kwa 'kutowaleta wakazi pamoja'.

Noor ameonyesha azma yake ya kuwania nyadhfa ya kiti cha mwakilishi wadi katika wadi ya Flamingo, huku akitaja eneo hilo kama wadi inayohitaji maendeleo zaidi kama vile vyuo vya anuwai pamoja na ajira kwani wakazi wengi katika eneo hilo ni vijana wasiokuwa na ajira.

Gikaria naye alisema kuwa Nakuru ni mji ulio na makabila yote na hangependa yatokee yaliyotukia mwaka wa 2007/2008, na kwa hivyo amani ndio jambo linalomsukuma kila kuchao. 

Gikaria amewaomba wananchi kudumisha amani msimu huu wa krismasi na mwaka mpya.