Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Hospitali ya Portreiz katika wadi ya Airport eneo bunge la Changamwe imepata ufadhili wa fedha za kusaidia kununua dawa pamoja na kuimarisha huduma zake.

Ufadhili huo kutoka nchini Ujerumani unatarajiwa kutatua tatizo la ukosefu wa dawa ambao umekuwa ukishihidiwa kila mara wakaazi wanafika kupata matibabu.

Akiongea na mwandishi huyu siku ya Alhamisi afisini mwake, mwakilishi wa wadi hiyo Fadhili Mwalimu alisema kuwa wanatarajia kutekeleza mpango huo mwaka huu.

“Tumepokea ufadhili na jambo la kwanza la kuzingatia ni kununua dawa, na pia tutaijenga hospitali yetu iwe bora zaidi,” alisema Fadhili.

Mwakilishi huyo alisema Ujerumani pia imekubali kufadhili shule ya msingi pamoja na ile ya upili ya Mwijabu eneo hilo ambapo wanazindua mradi wa kuijenga upya kabla mwaka huu kukamilika.

“Hiyo ni mipango ya mwaka huu na tunataka kuijenga iwe shule ya kisasa ambapo hata wanafunzi watakuwa na mazingira mazuri ya kusomea,” aliongeza mwakilishi huyo.

Hospitali ya Portreiz inategemewa sana na wakaazi wa eneo bunge la Changamwe pamoja na viunga vyake ikizingatiwa kwamba ipo karibu zaidi na wakaazi hao.

Kwa muda wakaazi wa eneo hilo wamekuwa wakilalamika kutokana na kile wanachodai ni ukosefu wa dawa hospitalini humo pamoja na huduma duni za matibabu.

Taarifa ya kupatikana kwa ufadhili inakuja muda mfupi baada bunge la kaunti ya Mombasa kufunguliwa tena rasmi ambapo inatarajiwa kuanza vikao vyake Jumatatu hii ili kujadili hoja mbalimbali zinazohusu kaunti hiyo.