Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Maafisa wa polisi wa kaunti ya Nakuru wameihimiza idara ya mahakama kusaidia kukabiliana na pombe haramu kwa kuwatoza faini za juu na vifungo vikali kwa wale wanaopatikana na hatia hiyo.

Kamishina wa kaunti ya Nakuru Joshua Nkanatha alisema inasikitisha kuona kuwa biashara hiyo imeanza kurejea tena baada ya kampeni iliyozinduliwa na rais Uhuru Kenyatta ya kukabiliana nayo kukamilika.

Akizungumza katika shughuli ya kuvamia kituo kimoja cha upikaji chang’aa kilicho katika eneo la Mwariki, viungani mwa mji wa Nakuru, ambapo zaidi ya lita elfu tano za kangara zilinaswa, Nkanatha aidha alikariri kuwa wamepokea taarifa kuwa mumliki wa kituo hicho alikuwa mwendeshaji sugu wa biashara hiyo ambaye alikuwa amefikishwa mahakamani mara kadhaa.

Kwa upande wake, kamanda wa kitengo cha utawala Francis Kiraithe aliyeandamana na kamishina huyo alisema kuwa watafanyakazi na machifu na maafisa wa polisi kuhakikisha kuwa wanapata taarifa kuhusiana na biashara sawia.

Aidha, naibu kamishna wa divisheni ya manispaa ya Nakuru Catherine Njoroge aliyekuwa alisema njia mpya zimeanza kuvumbuliwa za kuuza pombe hiyo haramu nchini licha ya shughuli ya kukabiliana na pombe hiyo kuendelezwa kote nchini.