Wakazi wa Mombasa wanaitaka idara ya polisi kote nchini kuhakikisha inakabiliana na makundi yote ya kugaidi ili amani na utulivu upatikene.
Wakizungumza na mwanahabari huyu siku ya Jumapili, wakazi hao wamesema kuwa vijana wengi wanajihusisha na visa vya ugaidi nchini pasi kujali maisha ya wengine.
Mohamed Salim, mkazi wa Mtwapa alisema kuwa vijana wanaojiuhusisha na ugaidi wanafaa kukabiliwa vilivyo kisheria ili visa vya uvamizi kupungua.
Hatua hii inajiri baada ya idara ya polisi kutoa picha za watuhumiwa watatu wa ugaidi ambao wanahusishwa na shambulizi la basi huko Mandera na Elwak pamoja na kuhusishwa na kutaka kufanya mashambulizi katika majengo ya bunge.
Inspekta mkuu wa polisi nchini Joseph Boinnet ametoa wito kwa wananchi kutoa habari kwa polisi kuhusu washukiwa hao, huku akitangaza zawadi ya hadi shilingi milioni 2 kwa atakayetoa taarifa kuwahusu.
Habari kutoka kwa kitengo cha ujasusi ni kwamba washukiwa hao wanashirikiana na wafuasi wa kundi la Alshabaab kufanya mashambulizi.
Boinnet amewahimiza wakenya kuwa makini kwani washukiwa hao wanaaminika kuwa na silaha hatari.
Abdullahi Issak Diyat ambaye ni mshukiwa wa kwanza inasemekana kuwa alihusika katika shambulizi la basi la Makkah Novemba mwaka wa 2014 ambapo watu 28 waliaga dunia.
Pia alihusika katika kuuwawa kwa watu katika timbo huko Mandera mwaka huo huo.
Mshukiwa mwengine Idriss Issack Ismail anasakwa kwa makosa sawia na hayo huku mshukiwa watatu Ahmed Uweys anasemekana alijiunga na kundi la Al Shabaab kama mpiganaji.