IEBC iliandaa kikao na viongozi wa mrengo pinzani wa CORD siku ya Jumanne.
Sababu yah ii ilikuwa kusikiliza malalamishi ya mrengo huo kuhusu usajili wa wapiga kura. Mkutano huo uliaandaliwa katika afisi za IEBC jijini Nairobi siku moja tu baada ya usajili wa wapiga kura kuzinduliwa rasmi.
Miongoni mwa tetesi zilizoibuliwa na CORD ni mapendeleo katika usambazaji wa mitambo ya BVR ambapo kwa mujibu wao IEBC inapendelea sehemu zinazokisiwa kuwa ngome kuu za mrengo tawala wa Jubilee.
Viongozi hao pia walilalamika kuwa tume ya IEBC ina njama ya kuwafungia nje baadhi ya wafuasi wa mrengo wa CORD kwenye shuguli ya kuwasajili wapiga kura.
Hata hivyo vigogo hao, Raila Odinga, Kalonzo Musyoka na Moses Wetangula walidhibitisha kuwa wameafikiana kuwa tume ya IEBC itashughulikiwa malalamishi yao.
‘‘Tume ya IEBC imetuahidi kuwa itafanya uchunguzi zaidi kuhusu masuala tuliyowasilisha na watafanya mabadiliko iwapo kuna tatizo lolote ili kuhakikisha kuwa usajili wa wapiga kura unaendelezwa kwa njia inayofaa na ya usawa,’’ alisema Odinga.
Viongozi hao walisema kuwa iwapo tume ya IEBC haitatimiza ahadi yake , viongozi watazidi kuishurutisha hadi marekebisho hayo yatapofanywa.
‘‘Iwapo hawatatimiza walioyasema tutarejea hapa ofisini kwao kuwaeleza jinsi ya kutekeleza masuala kwa njia bora,’’ alisisitiza Wetangula.