Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Kioja kilizuka Jumatatu jioni katika mtaa wa Barnabas viungani mwa mji wa Nakuru, wakati jamaa mmoja mwenye umri wa makamo alipatikana na wenyeji akitafuna nyasi mithili ya ng’ombe.

Haijabainika jamaa huyo kama ametoka katika eneo hilo la Pipeline ama alitoka mbali, huku umati mkubwa wa watu ukijitokeza kujionea kisanga hicho cha kipekee ambacho mara kwa mara huhusishwa na wizi ama uhalifu.

Juhudi za wakaazi hao kumhoji ziliambulia patupu, kwani hakuweza kunena lolote ila alisalia kimya kama maji yatuliavyo mtungini, huku akitafuna nyasi nao umati ukimduwaa.

“Hakuweza kujibu anatoka wapi, anaitwa nani ama ni kwa nini anakula nyasi. Tulidhania kwamba amefanyiwa mazingaombwe,”Geoffrey Maina alisema.

“Nyasi yote aliyokuwa amekula kabla ya kuchukuliwa na polisi, inaweza kufika kilo tatu ama nne ikipimwa. Mimi nilimhurumia kwa sababu niliona huo sio ugonjwa, ni kama amerogwa,” Monica Njeri alisema.

Hata hivyo polisi kutoka kituo cha Mwariki waliarifiwa na kumchukua jamaa huyo, ambapo yaarifiwa alipelekwa hospitalini kaba ya uchunguzi kamili.