Wito umetolewa kwa kila mmoja kwenye jamii kuvalia mavazi ya heshima ili kuzuia visa vya unajisi na ubakaji hasa katika jimbo la Kisumu.
Mkurugenzi mkuu wa shirika lisilo la kiserikali la Hope Link jijini Kisumu Radido Dooso alisema kuwa ni muhimu kwa kila mmoja kuzingatia maadili ikiwemo kuvalia mavazi yenye heshima, ili kuzuia maovu yanayozidi kukithiri katika jamii.
“Baadhi ya matatizo ya kijamii tunayoshuhudia kwa sasa kama ubakaji na unajisi yanachangiwa kwa asilimia kubwa na mavazi duni ambayo yanaendelea kujipatia umaarufu hasa miongoni mwa wanawake. Iwapo tutakabiliana na uwepo wa mavazi haya, basi matatizo hayo yatakabiliwa,” alisema Dooso jijini Kisumu siku ya Jumatatu.
Dooso alitoa changamoto kwa viongozi wa kidini kutumia nafasi zao kwenye jamii kuchochea na kupalilia maadili mema yatakayokuza kizazi cha baadaye chenye heshima na maadili.
Aliwahimiza wazazi kuwa katika mstari wa mbele kuwahimiza watoto wao kuvalia mavazi yenye heshima, akisisitiza kuwa jamii kwa ujumla ina jukumu la kuhakikisha kuwa maadili yanazingatiwa nyakati zote.