Jamii ya waumini wa dini ya Kiislamu katika kaunti ya Kisumu inalalamikia kubaguliwa katika zoezi la kuwasajili wapiga kura linaloendelea kote nchini.
Akizungumza katika Kongamano la Kisumu Women and Leadership Caucus, mwakilishi mteule katika bunge la kaunti ya Kisumu Farida Salim amesema waislamu wameishia kukumbana na changamoto wanapohitaji kupata vitambulisho vya kitaifa ambayo ni tiketi ya kusajiliwa kama mpiga kura.
Farida anasema changamoto hizo zinaikosesha motisha jamii hiyo na huenda idadi ya wapiga kura wanaotarajiwa kusajiliwa ikakosa kuafikiwa.
‘’Wengi wao wanakosa kitambulisho na unajua bila kitambulisho ni vigumu sana kwa yeyote kujiandikisha kuchukua kura,’’ alisema Bi Salim.
Aliongeza kuwa baadhi yao ambao walijiandikisha kupewa vitambulisho vya taifa zaidi ya miaka 2 iliyopita na hadi kufikia sasa serikali haijawapa vitambulisho vyao.