Mbunge wa eneo bunge la Borabu kaunti ya Nyamira Ben Momanyi ameomba jamii ya Kipsgis na ile ya Kisii mpakani Isoge kuishi kwa amani ili kuruhusu maendeleo katika maeneo hayo.
Wito huo umetolewa baada ya jamii hizo mbili kuwa na tofauti kila wakati huku jamii ya Kipsgis ikidaiwa kuiba mifugo kutoka jamii ya Kisii jambo ambalo limeleta utata kati ya jamii hizo mbili kwa muda mrefu.
Kulingana na Mbunge Momanyi ambaye alizungumza katika eneo bunge lake la Borabu alisema kuwa mizozo ambayo hushuhudiwa kati ya jamii hizo mbili hurudisha maendeleo nyuma zaidi huku akiomba kuishi kwa amani kuruhusu maendeleo kuendelea
“Hakuna haja kuishi tukiwa maadui maana uadui hurudisha maendeleo nyuma katika sehemu tunayoishi,” alisema Momanyi.
“Naomba tuishi kwa amani na tujitenge na uharibifu wa kila aina ili maendeleo yawe kwetu,tufanye biashara pamoja tujiinue kimaisha na kiuchumi kama taifa moja,” aliongeza Momanyi.
Kwa upande wa wakaazi wa Borabu wakiongozwa na Peterson Nyakwara waliomba serikali kuchunguza wizi wa ng’ombe ambao unaendelea kushudiwa katika eneo hilo huku jamii ya Kipsigis ikishukiwa kuhusika kwa wizi huo wa mifugo.