Jamii za Pokomo na Orma katika Kaunti ya Tana River wameombwa kujitenga na viongozi wachochezi wanaotumiwa na baadhi ya mabwenyenye kuwatenganisha kisiasa na kikabila ili kunyakua ardhi zao.
Mwenyekiti wa Chama cha Mzalendo nchini Abdallah Bwanamaka amesema kuwa kuna baadhi ya viongozi wa kisiasa wanaotumiwa na mabwenyenye kuzigonganisha jamii hizo ili kuzua vurugu, na kusababisha jamii hizo kuhama maeneo hayo na ardhi zao kunyakuliwa na mabwenyenye hao.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Ijumaa, Bwanamaka alisema kuwa kama viongozi wa eneo hilo, kamwe hawatakubali kuona jamii hizo mbili zikilumbana kwasababu ya baadhi ya viongozi wachochezi.
Bwanamaka alisema kuwa wanawachunguza baadhi ya viongozi fulani na ripoti kamili itawasilishwa kwa maafisa wa usalama ili viongozi hao kuchukulia hatua.
Aliongeza kuwa sio vyema kwa jamii mbili kulumbana huku wengine wakifurahia na kupata fursa ya kunyakua ardhi zao.
“Kama viongozi wa jamii hizi mbili kamwe hatutakubali kuona baadhi ya viongozi wakizigonganisha jamii hizi kwa manufaa yao binafsi. Lazima hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya watu kama hao ili kaunti ya Tana River iwe na amani,” alisema Bwanamaka.
Aidha, aliahidi kuzuru kaunti hiyo hasa mashinani kunakodaiwa kulengwa sana na viongozi hao wachochezi, ili kuhakikisha kuwa wanazihamasisha jamii hizo kujitenga na viongozi kama hao na kudumisha amani.