Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mnazi ni mojawapo ya miti inayostawi katika eneo la Pwani na huwafaa na kuwakidhi wakaazi kwenye shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Baadhi ya wakaazi katika Kaunti ya Mombasa na Kaunti zingine za Pwani hutumia mmea huo kupata fedha za karo za watoto wao na vile vile kunufaika katika mahitaji ya nyumbani.

Huu ni mti ambao una manufaa mengi sana, ikilinganishwa na miti mingine inayokuzwa nchini.

Yafuatayo ni bidhaa zinazotokana na mti huu na manufaa mengineyo;

Nazi: Tunda la mnazi ambalo limekomaa kabisa na lenye ngozi ngumu. Tunda hilo huwa jeupe.

Tui: Maji meupe ambayo hutokana na nyama nyeupe ya nazi iliyokunwa. Tui hutengeneza maziwa ya nazi au uji baada ya kuchujwa.

Madafu: Aina ya tunda la nazi ambalo halijakomaa na maji yake hutumiwa na wakaazi kama dawa ya kusafisha figo.

Makuti: Haya ni matawi ya mnazi na hutumiwa kufanikisha shughuli mbalimbali ikiwemo kuezeka nyumba.

Ganda: Ngozi ya nje ya nazi ambayo hutumiwa kutengeneza vifaa kama vile vikombe.

Makumbi: Aina ya nyuzi ambazo huwa nje ya nazi na hutumiwa pamoja na sufi kutengeneza aina fulani ya zulia na kujalizia magodoro.

Mnazi: Aina ya pombe ambayo hutengenezwa kutokana na maji ya nazi na hupendwa na wakaazi wa eneo la Pwani, hasa nyakati za sherehe maalumu.

Pamoja na manufaa hayo, mti huo hutumiwa kujenga nyumba, huku mizizi yake ikitumiwa kutibu aina fulani ya maradhi.

Mti huo pia huzaa matunda ambayo huzalisha na kutengeneza mafuta ya nazi.