Gavana wa Kaunti ya Mombasa ambaye pia ni naibu kiongozi wa chama cha ODM Hassan Joho amempongeza mgombea wa kiti cha ubunge cha eneo la Malindi kwa tikiti ya ODM.
Joho amempongeza William Mtengo aliyeteuliwa kupeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mdogo unaotarajiwa kufanyika tarehe Machi 7, 2016.
Akiongea alipokutana na kundi la wanawake katika eneo la Kakuyuni Kilifi siku ya Jumatatu, Gavana Joho alitoa matumaini yake kwa mgombea huyo na kuhakikishia wakaazi hao kwamba chama hicho kitaibuka na ushindi.
“Mimi kama naibu mwenyekiti wa chama ningependa kupongeza mgombea wetu na pia watu wa Malindi kwani wamekuwa wakakamavu na wenye subira.” alisema Joho.
Gavana huyo pia aliwashukuru wale wanachama wote walioonyesha utulivu na kukubali kushindwa katika uteuzi akisema kuwa hiyo ni hali ya kisiasa na kwamba chama hicho kitasalia kuwa dhabiti katika eneo hilo.
Kiti cha ubunge cha Malindi kilisalia wazi baada ya Rais Uhuru Kenyatta kumteua aliyekuwa mbunge wa eneo hilo Dan Kazungu kama waziri mpya wa madini.
Uchaguzi huo mdogo wa mwezi Machi umeibua hisia tofauti hasa wakati Rais Uhuru alipozuru eneo hilo wakati wa ziara yake ndefu aliyoifanya Pwani.
Baadhi ya viongozi wa upinzani walidai kwamba ziara hiyo ilikuwa njia ya kupigia debe mgombezi wa chama cha JAP.