Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho ametangaza azimio lake la kuwania kiti cha urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2022.
Akihutubia viongozi wanawake wa chama cha ODM kutoka mashinani huko Kakuyuni kaunti ndogo ya Malindi siku ya Jumatatu, Joho alisema mpwani anayo haki na uwezo wa kuwania kiti cha urais, hivyo kunahaja ya Wapwani kuungana na kuchukua uongozi wa nchi.
Joho amewataka viongozi wa Pwani kumuunga mkono kwenye uchaguzi huo wa mwaka 2022 ili kupata nafasi ya kuongoza taifa hili na kuwa mpwani wa kwanza kuongoza nchi.
Aidha, aliongeza kuwa yuko na uwezo wa kuongoza na kuboresha uchumi wa taifa hili iwapo atachaguliwa kuwa rais.
“Miradi iliyoanzishwa na serikali ya Jubilee sawia na ahadi za miradi ya maendeleo zilizotolewa na Rais Kenyatta wakati wa ziara yake hapa Pwani ni siasa. Wananchi hawapaswi kusherehekea kwani miradi hiyo ni haki yao kikatiba,” alisema Joho.
Amewataka viongozi wa Pwani kutokubali kununuliwa na muungano wa Jubilee.