Mbunge wa Mvita Abdulswamad Shariff Nassir amekosoa vita vya maneno vinavyoendelea kati ya Gavana wa Kaunti ya Mombasa na Seneta wa Kaunti hiyo Hassan Omar na kusema kuwa wawili hao wanapaswa kufanya kazi kwa pamoja.
Akizungumza katika eneo bunge lake la Mvita mjini Mombasa siku ya Jumamosi, Abdulswamad alisema kuwa japo wawili hao wana fikra tofauti za kisiasa na kiuongozi, malumbano yao yanatatiza uongozi wa Kaunti hiyo na maendeleo kwa wananchi.
Mbunge huyo aliwataka wawili hao kuafikiana kuhusu maswala muhimu ya kimaendeleo katika kaunti hiyo ili wakazi wa kaunti ya Mombasa wapate huduma bora badala ya kushghudia siasa za mabishano zisizokuwa na msingi wowote bali kutafuta ubabe wa kisiasa.
“Tunawaomba viongozi hao wawili kuungana na kuwatumikia wakaazi wa kaunti ya Mombasa badala ya wao kuzozana kila uchao kwa misingi ya kisiasa kwani uhasama huo kamwe hautajenga uchumi wa kaunti bali kubomoa," alisema mbunge huyo.
Aidha aliwataka wakazi wa Kaunti hiyo ya Mombasa kuwachagua viongozi wanaostahili kuimarisha kaunti hiyo kimaendeleo pindi uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2017 utakapowadia.
“Wakati umefika sasa kwa wakaazi wa kaunti kuwachagua viongozi waadilifu na wenye nia ya kubadili uongozi na kuleta maendeleo kwa jamii ya Mombasa, eneo la pwani na taifa zima kwa jumla hivyo basi jitokezeni kwa usajili wa wapiga kura ndio mshiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu," aliongeza Abdulswamad.
Kauli ya Mbunge huyo inajiri siku chache tu baada ya wabunge wa bunge la Kaunti ya Mombasa wakiongozwa na Spika wa bunge hilo Thadius Rajwayi kumkashfu vikali Seneta wa Kaunti ya Mombasa.