Share news tips with us here at Hivisasa

Wachanganuzi wa maswala ya kisiasa katika eneo la Pwani wamelitaka jopo lililoteuliwa kumchunguza Jaji Philip Tunoi, linaloongozwa na Jaji Shared Rao, kuhakikisha kuwa ukweli dhidi ya madai hayo yanawasilishwa wazi, baada ya ripoti ya uchunguzi wao kukamilika.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatano, Wakili Johnson Muchiri, alisema kuwa wako na imani na jopo hilo na kulitaka kuweka wazi ukweli dhidi ya madai kuwa Jaji Philip Tunoi alipokea rushwa ya shilingi milioni 200 kutoka kwa Gavana wa Kaunti ya Nairobi Evans Kidero, ili kutupilia mbali kesi iliyokuwa imewasilishwa mahakamani na mpizani wake Ferdinard Waititu kuhusu uchuguzi wa mwaka wa 2013.

“Kama wachanganuzi wa kisiasa katika eneo la Pwani tuko na matumaini na Jopo liliteuliwa na Rais Kenyatta kuchunguza kashfa zinazomkabili Jaji Tunoi. Tunaliomba jopo hilo kutoegemea upande wowote na kutoa ripoti kamili kuhusu kashfa hiyo,” alisema Muchiri.

Aidha, Muchiri alikosoa kucheleweshwa kwa kuteuliwa kwa jopo hilo, na kudai kuwa Rais Uhuru Kenyatta huenda akawa ana malengo ya kuficha ukweli kuhusiana na sakata ya ufisadi inayomuandama jaji huyo.

Alisema kuwa Rais Kenyatta alichelewesha kuteuliwa kwa jopo hilo licha ya mahakama kuu nchini kumpa muda wa siku 14 kutekeleza swala hilo.

Jopo hilo lililoteuliwa na Rais Kenyatta litaongozwa na Jaji Sharad Rao, huku wanachama wakiwa Roseline Korir, Judith Guserwa, James Kaberere Gacoka, Mr Abdirashid Abdullahi Hussein na George Munji Wakukha.