Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Viongozi wa chama cha Jubilee wametangaza kukubali kushindwa kwenye uchaguzi mdogo wa Malindi uliofanyika siku ya Jumatatu.

Wakiongozwa na Mwenyekiti wa wabunge wa Pwani Gideon Munga'ro viongozi hao walisema kuwa uchaguzi huo umekuwa wa huru na haki na wamekubali kushindwa katika uchaguzi huo na kuwasihi wakaazi wa eneo bunge la Malindi kukubali matokeo hayo.

Mung'aro ambaye pia ni Mbunge wa Kilifi Kazkazini alisema kuwa chama cha Jubilee kinajiandaa vyema katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka wa 2017, na wanamatumani ya kushinda uchaguzi huo kwani watarekebisha mahala walipokosea.

Mungaro aliipongeza Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini IEBC, kwa kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika vyema bila ya hitilafu yoyote, licha ya kukumbwa na changamoto za baadhi ya watu kujaribu kuwahonga baadhi ya wakaazi.

"Tumefurahia jinsi Tume ya IEBC ilivyoendesha uchaguzi huo pamoja na jinsi maafisa wa usalama walivyohakikisha kuwa usalama unaimarisha katika eneo hilo ili uchaguzi huo kuwa wa huru na wazi. Matokeo yaliyotolewa tumekubali kama Jubilee na tunawaomba wakaazi kuwa watulivu na kudumisha amani,” alisema Mung'aro.

Uchaguzi huo ulimpa ushindi Willy Mtengo kwa asilimia 58 huku mpinzani wake Phillip Charo akipata asilimia 34. Sasa kinachosubiriwa ni kuapishwa kwa Willy Mtengo kuwa Mbunge wa Malindi.