Share news tips with us here at Hivisasa

Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Evans Achoki amewaonya maafisa wa usalama katika kaunti hiyo dhidi ya kujihusisha na visa vya ufisadi.

Kauli yake inajiri baada ya visa vya ufisadi kuripotiwa kuongeza katika maeneo ya Old Town, Kaunti ya Mombasa.

Akizungumza katika ziara yake ya kwanza katika maeneo ya Old Town, Kamishna Achoki alisema kuwa sharti maafisa wa usalama waasi ufisadi na wajitambulishe kupitia nambari zao za kazi wakati wa utendakazi wao katika maeneo mbalimbali, ili haki za wakazi zipate kudumika.

Achoki pia aliwahimiza wazazi kuendeleza malezi bora na kuendeleza elimu katika viwango mbalimbali ili kupunguza visa vya utovu wa nidhamu, uraibu wa dawa za kulevya na makundi mbalimbali ya kigaidi.

Aidha, Achoki alisema kuwa katika maeneo ya Mombasa, idadi ndogo ya vijana, kina mama na watu wanoishi na ulemavu wamefaidika kutokana na mikopo ya serikali.

Kulingana na Achoki, kujihusisha na mikopo ya biashara itawawezesha kina mama, vijana na watu wanaoishi na ulemavu kuimarika na kuboresha uchumi nchini.

Vile vile, kamishna huyo amewataka wakazi wa Mombasa kutoa nambari zao za simu wakati wa kujiandikisha kupata vitambulisho ili waweze kujulishwa wakati kitambulisho kimetoka.

Alisema hatua hiyo itasaidia kupunguza idadi ya vitambulisho vilivyokosa kuchukuliwa baada ya kutayarishwa.

Kwa mujibu wa Kamishna huyo, wakazi wa Mombasa wataweza kupata vitambulisho licha ya changamoto mbalimbali ili kuwawezesha kufaidi miradi ya ugatuzi nchini, kudumisha amani na kuboresha uchumi nchini.

Hata hivyo amewataka wakazi wa Mombasa kushirikiana ili kusaidia kuendeleza usalama na kudumisha amani katika maeneo ya Mombasa.