Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wafanyibiashara katika Soko la Kongowea, Marikiti na Mwembe Tayari mjini Mombasa wamemtaka Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho kuhakikisha anakarabati masoko hayo ili kuboresha shughuli za kibiashara.

Wafanyibiashara hao walisema kwamba kuwepo kwa mazingira duni ya masoko hayo pamoja na kuwepo na mirundiko ya taka karibu na masoko hayo kumechangia kuwepo na biashara duni hali ambayo inachangia kudorora kwa uchumi wa kaunti.

Wakiongozwa na Katibu wa Chama cha Wafanyibiashara wa Soko la Kongowea Peter Nyaga, wafanyibiashara hao walisema kuwa Gavana Joho anapaswa kutenga bajeti ya kukarabati masoko makuukuu ili kuwekeza vyema katika masuala ya biashara.

“Tunamuomba Gavana Joho kuhakikisha kuwa masoko ya Mombasa yanafanyiwa ukarabati hususan Soko la Kongowea, Marikiti na Mwembe. Masoko haya tayari yamehudumu kwa muda bila ya kufanyiwa ukarabati,” alisema Nyaga siku ya Ijumaa katika mkutano wa wafanyibiashara mjini Mombasa.

Wafanyibiashara hao wameshikilia kuishinikiza serikali ya Kaunti ya Mombasa ili kuona kuwa wanapata mazingira bora ya kibiashara na kuwekeza zaidi katika kukuza uchumi wa Kaunti ya Mombasa na nchi na kwa jumla.