Uchaguzi mkuu wa mwaka 2017 unakaribia huku kampeni za mapema zikianza kuonekana katika maeneo kadhaa kote nchini.
Baadhi ya viongozi wanaonekana kuvihama vyama vyao na kujiunga na vyama tofauti.
Chama cha ODM huenda kikakabiliwa na tishio la kumpoteza mmoja wa viongozi wake baada ya Naibu Gavana wa Kaunti ya Mombasa Bi Hazel Katana kutangaza kuunga mkono chama kipya cha Jubilee.
Akiongea katika kampeni za uchaguzi huko Malindi, Bi Katana alikosoa chama cha ODM kwa madai kwamba hakina manufaa yoyote kwa Wapwani licha ya kujigamba kuwa Pwani ni ngome yake.
Bi Katana aliongeza kuwa ODM imekuwa kwa upinzani muda huo wote lakini hakuna faida yoyote watu wa Pwani wanayopata kutokana na hilo.
“Tumekuwa kwa upinzani miaka hiyo yote lakini hakuna kitu chochote tunachoweza kuonyesha kuwa tumefaidi,” alisema Bi Katana.
Sasa kauli hiyo ya naibu gavana wa Mombasa inazua maswali katika eneo hilo kuhusu hatua za viongozi wa upinzani kumezea mate upande wa serikali.
Matamshi yake yanakuja baada ya mbunge wa Likoni Masoud Mwahima kutangaza kukihama chama cha ODM na kujiunga na Jubilee wakati Rais Uhuru Kenyatta alipozuru eneo hilo.