Serikali ya Kaunti ya Uasin Gishu imepanga kufungua zahanati 18 zilizo katika maeneo tofauti katika kaunti hiyo.
Mkuu wa Idara ya Afya Bw Sillas Boit alisema hatua hiyo itasaidia katika kupunguza msongamano wa wagonjwa katika hospitali na pia kuimarisha utenda kazi katika idara hiyo ya afya.
Akizungumza mjini Eldoret, Boit alisema kwamba zahanati hizo zilizoko katika sehemu tofauti katika kaunti hiyo tayari zimejengwa na kwa sasa zinangoja tu vifaa vitakavyotumika kabla ya kufunguliwa rasmi.
“Ujenzi wa zahanati hizo umekamilika na tunalolipangia ni kuweka vifaa muhimu vitakavyo hitajika kabla ya kufunguliwa kwa zahanati hizo. Mradi huu utawafaidi wakazi wote wa kaunti hii kwani kila kaunti ndogo ina hospital mpya,” alisema Boit.
Boit alisema kwamba wahudu wa afya 362 wanatarajiwa kupata kazi katika sekta hiyo ya afya kabla mwisho wa mwezi ujao.
“Chumba cha kufanyia utafiti na kupima magonjwa tofauti kitatengwa ili kuhudumia Kikundi cha hospitali mbili au tatu. Usajili unaoendelea sasa utahakikisha kwamba kaunti hii imewaajiri wahudumu 362 katika wizara ya afya ili kufanya kazi katika zahanati hizo mpya,” alisema Boit.
Aidha, kaunti hiyo imejihusisha na shuguli ya kuwapa motisha wafanyikazi wote na hasa wahudumu wa afya.
Kauti hiyo imetenga Sh10,000 kwa kila mhudumu wa afya ili kushughulikia mambo tofauti na hasa ununuzi wa sare mpya.
Kaunti hiyo pia inaendeleza ukufunzi wa wahudumu hao katika vitengo mbali mbali.