Baada ya soko jipya kufunguliwa katika eneo la Tombe kaunti ya Nyamira, serikali ya kaunti hiyo imehimizwa kuweka mradi wa maji na kujenga vyoo katika soko hilo.
Kulingana na mwakilishi wa wadi ya Manga, Peter Maroro maji na vyoo yanastahili kuwekwa ndiposa soko hilo liwe kamilifu.
Akizungumza katika soko hilo la Tombe, Maroro aliomba serikali ya kaunti hiyo kujaribu kila iwezalo kuhakikisha mahitaji hayo muhimu yameshughulikiwa haraka ili kuleta afueni kwa wafanyibiashara wa soko hilo.
“Naomba maji yaweze kuunganishwa katika soko hili,” alisema Maroro.
“Pia naomba vyoo vijengwe ili kusaidia wafanyibiashara wetu wanapoendelea kufanya shughuli zao za kibiashara,” aliongeza Maroro.
Matamshi hayo yaliungwa mkono na wafanyibiashara wa soko hilo huku wakisema yale ambayo wamekosa ni maji na vyoo.