Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Serikali ya kaunti ya Kisii imeombwa kuingilia kati ujenzi wa hospitali ya Mwamogesa iliyoko eneo bunge la Kitutu Chache kusini ili kukamilisha ujenzi wa hospitali hiyo.

Hii ni baada ya ujenzi wa hospitali hiyo kuanzishwa zaidi ya miaka 13 iliyopita bila kukamilika, huku ujenzi huo ukiachiwa njiani.

Ujenzi huo ulikuwa chini ya uongozi wa mbunge wa eneo bunge hilo la Kitutu chache kusini Richard Onyonka, na mradi huo ukakwama baada ya sekta ya afya kugatuliwa.

Wakizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatatu katika eneo hilo la Mwamogesa, wakazi wa eneo hilo wakiongozwa na Geoffrey Tinega waliomba serikali ya kaunti ya Kisii kuingilia kati na kuwasaidia kukamilisha ujenzi huo ili hospitali hiyo kuanza kutumika.

Kuligana na wakazi hao huwa wanasumbuka kutafuta matibabu katika hospitali ya rufaa na mafunzo mjini Kisii kwa kutembea mbali kutafuta matibabu hayo.

“Tunaomba serikali ya kaunti yetu ya Kisii kutoa msaada kwetu maana tumesumbuka kwa kutokuwa na hospitali katika eneo hili kwa mda mrefu maana hospitali ambayo ingetusaidia iliachiwa njiani bila kukamilishwa kujengwa,” alisema Tinega .

Aidha, mbunge Onyonka alilaumiwa kwa kutojali maslahi ya wakazi wa eneo hilo kwa kutokamilisha ujenzi wa hospitali hiyo na kumwomba kukarabati barabara za eneo hilo ambazo hazipitiki.