Serikali ya Kaunti ya Nyamira imeombwa kutoa usaidizi kwa watoto mayatima na familia zisizojiweza wakati huu wa sherehe za krismasi na mwaka mpya, ili nao waweze kusheherekea kama watu wengine.
Akizungumza siku ya Jumatatu mjini Nyamira, naibu mwenyekit wa Chama cha Maendeleo ya Wanawake katika kaunti ya Nyamira Jerusha Momanyi, alisema kuna haja ya mayatima na familia zisizojiweza kupata msaada wa kifedha au bidhaa muhimu kama vyakula ili kuwawezesha kusheherekea krismasi.
Momanyi alisema kuwa familia nyingi huwa hazipati fursa ya kusheherekea krismasi kufuatia ukosefu wa pesa.
Aidha, aliomba wahisani wema na akina mama katika kaunti ya Nyamira kuwa katika mstari wa mbele kutoa usaidizi msimu huu wa likizo.
“Naomba serikali ya kaunti yetu kutoa usaidizi kwa mayatima na familia zisizojiweza ili waweze kufurahia krismasi kama watu wengine,” alisema Momanyi.
Aliongeza, “Wahisani na akina mama naomba tujitolee kwa kuwapa mayatima vyakula. Hakuna haja ya kujifurahisha peke yetu na kuacha wengine kando.”