Share news tips with us here at Hivisasa

Kongamano la wafanyibiashara kutoka mataifa mbalimbali na sehemu zingine za taifa la Kenya limeanza rasmi hii leo katika Chuo kikuu cha Kisii, mjini Kisii.

Kongamano hilo ambalo limewaleta wafanyibiashara kutoka mataifa mbalimbali pamoja, litaandaliwa kwa siku tatu hadi siku ya Jumamosi.

Lengo la kongamano hilo ni kuhakikisha wananchi wanawekeza zaidi kwa biashara ili kujiendeleza na kuinua uchumi wa kaunti na taifa la Kenya kwa jumla.

Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatano mjini kisii, Gavana wa Kaunti ya Kisii James Ongwae aliwakaribisha wafanyibiashara wote watakao hudhuria kongamnao hilo.

Ongwae alisema kuwa lengo la kuwaleta pamoja wafanyibiashara hao ni kutoa mafunzo kuhusu jinsi ya kujiendeleza kupitia biashara na kuwekeza katika biashara.

Gavana huyo alisema wageni kutoka mataifa mbalimbali ikiwemo China, Marekani, Ujeromani, Afrika kusini, Uingereza, Israeli, India na mataifa mengine watahudhuria kongamano hilo.

Aidha, Ongwae alisema kuwa Rais Uhuru Kenyatta atafika kwa kongamano hilo siku ya Jumamosi ili kufunga mkutano huo rasmi, na kuomba wengi kufika katika chuo hicho kujionea na kupokea mafuzo ambayo yatawasaidia kujiinua kibiashara.