Chama cha Mawakili humu nchini, LSK kimetoa onyo kufuatia usemi wa Rais Uhuru Kenyatta kudinda kuteua jopo la kumchunguza jaji wa mahakama ya juu Philip Tunoi.
Akigusia barua iliyowasilishwa siku ya Jumatatu kwa Jaji Mkuu Willy Mutunga na mwenyekiti wa tume ya huduma kwa mahakama nchini, JSC kupitia kwa katibu wa baraza la mawaziri, Joseph Kinyua alitoa sababu za rais kukataa kuunda jopo la kumchunguza jaji Tunoi.
Mwenyekiti wa LSK, Eric Mutua alisema kwamba kutoteuliwa kwa jopo hilo kutapelekea Tunoi kutochunguzwa kama ilivyopendekezwa na JSC.
Mutua aidha aliongeza kuwa iwapo Rais hatatekeleza jukumu hilo atakuwa anakiuka sheria.
" Tunataka kumkumbusha rais kuhusu kifungu cha katiba kwani anaweza ondolewa mamlakani na bunge kwa kukiuka katiba," Mutua alisema.
Alikosoa barua ya Joseph Kinyua iliyosema kuwa rais alikataa kuteua jopo hilo kwa sababu Tunoi ana kesi ya rufaa mahakamani ambapo anapinga umri wake wa kustaafu.
JSC iliwasilisha ombi kwa rais la kumtaka ateuwe jopo la kumchunguza Tunoi baada ya ushahidi kupatikana kuhusu madai ya Tunoi kupokea hongo kutoka kwa Kidero kumpendelea katika kesi ya kupinga kuchaguliwa kwa Kidero kama gavana mwaka wa 2013.