Share news tips with us here at Hivisasa

Maafisa wa afya katika Kaunti ya Nyamira wamepata dawa zinazo nakisiwa kuibiwa kutoka Hospitali Kuu ya Kaunti ya Nyamira.

Akizungumza baada ya msako katika maduka ya kuuza dawa kule Nyansiongo, Mkurungenzi katika Idara ya afya kwenye serikali ya kaunti hiyo Douglas Bosire alisema kuwa idara yake itaendelea na msako huo hadi maafisa wanaoiba dawa za umma watakapo asi tabia hiyo.

"Hatuwezi tukasitisha msako huu kwa kuwa tayari tushawaonya wahusika na sharti raslimali za umma ziheshimiwe. Wanaofikiria kuwa watajitajirisha kwa kuiba dawa za wananchi wafahamu kuwa hawana nafasi yakutekeleza wizi huo hapa Nyamira," alisema Bosire.

Bosire alisema kuwa idara yake itashirikiana na maafisa wa polisi ili kuhakikisha kuwa waliokuwa wakiuza dawa hizo za wizi wanakabiliwa kisheria.

"Sharti tuhakikishe kuwa sheria zinazingatiwa na lazima idara yangu ishirikiane kikamilifu na maafisa wa polisi kuhakikisha kuwa wenye maduka yaliokuwa yakiuza dawa hizo watafikishwa mahakamani kujibu mashtaka. Ninawasihi wakazi muepuke kununua dawa zilizo na ilani ya serikali ya kaunti na mnapo ona hilo, muwe tayari kupiga ripoti kwa maafisa wa polisi,” alisema Bosire.