Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mwenyekiti wa wahudumu wa matatu mjini Kisii, Okong’o Mose, amewataka madereva wa matatu kufuata na kuzingatia sheria za kuegesha magari.

Akizungumza siku ya Jumatano katika kituo cha magari mjini Kisii, Mose aliwaomba madereva hao kufuata sheria zilizowekwa na kuzingatia utaratibu uliopo wa kuyaegesha magari hayo, pindi wanapoingia mjini.

Kulingana naye, madereva wanaovunja sheria hizo za kuegesha magari mara nyingi husababisha msongamano mjini humo, na hata kutatiza shughuli za usafiri kwa watumizi wengine wa magari.

Mose alisema kuwa kamwe hatowaruhusu madereva hao kuvunja sheria hizo.

“Naomba kila dereva azingatie utaratibu wa kuegesha magari ya matatu mjini Kisii kama njia moja ya kurahisisha kazi ya uchukuzi hapa Kisii,” alisema Mose.

Wakati huo huo, Mose aliwaomba maafisa wa trafiki kuhakikisha kwamba magari yote ya kubeba abiria yako katika hali nzuri kwa usalama wa wanaosafiri.

“Nawaomba wamiliki wa magari kuhakikisha magari yao yako katika hali inayostahili kabla ya maafisa wa trafiki kuyaondoa barabarani,” alisema Mose.

Aliongeza, “Ikiwa mtasusia kufanya hivyo, basi huenda magari yenu yaondolewe barabarani kwani tunahitaji sekta ya uchukuzi iimarike zaidi Kisii.”