Madereva wa matatu mjini Nakuru wameitaka Halmasharuri ya usafirishaji na usalama barabarani NTSA kuweka taa za trafiki katika mizunguko ya barabara ya KFA na Gate House mjini Nakuru.
Madereva hao walisema kuwa ukosefu wa taa hizo unapelekea msongamano mkubwa haswa nyakati za asubuhi na jioni.
Akizungumza siku ya Alhamisi, Mwenyekiti wa chama cha usafiri cha Bahama Sacco Nelson Githinji, alisema kuwa uwepo wa taa hizo utasaidia kumaliza misongamano inayoshuhudiwa mjini Nakuru na vilevile ajali katika mizunguko hiyo miwili.
Githinji aliongeza kuwa taa hizo zitasaidia kuongoza madereva na watumizi wengine wa barabara wanaotoka na kuingia katikati mwa mji wa Nakuru na wale wanaotoka Nairobi kuelekea Eldoret.
“Kama tungekuwa na taa za trafiki katika mizunguko ya Gate House na KFA, hatungekuwa na msongamano mjini Nakuru. Msongamano huu unaletwa na ukosefu wa taa hizo kwa sababu kila dereva ana haraka ya kwenda na hataki kumruhusu mwengine apite, jambo ambalo linasababisha ajali nyingi haswa asubuhi na jioni,” alisema Githinji.
Alisema kuwa polisi wa trafiki wanapokosa kushika doria katika maeneo hayo mawili, shuguli hukwama mjini Nakuru kutokana na msongamano mkubwa.
“Nakuru inaendelea kupanuka na watu wanaendelea kuongezeka sawa na magari.Taa hizo za trafiki zitatufaaa tena sana kwa hivyo tunaomba NTSA kufikiria swala hilo na kulishugulikia,” alisema Githinji.