Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Afisi ya mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma imepata pigo baada ya mahakama kuu kudinda kufutilia mbali dhamana ya wasichana wanne wanaokabiliwa na madai ya ugaidi.

Akitoa uamuzi huo siku ya Jumatano, jaji Dora Chepkwony alisema kuwa uamuzi wa kupewa dhamana uliotolewa na mahakama ya chini ni wa halali na usawa kwa mujibu wa katiba.

Aidha, aliongeza kuwa kuwanyima dhamana washtakiwa hao itakuwa ni kukiuka uhuru na haki za washtakiwa hao kwa mujibu wa katiba, ikizingatiwa ombi lililowasilishwa na afisi ya mkurugenzi mkuu wa mashtaka halina sababu za kutosha kufutilia mbali dhamana hiyo.

Haya yanajiri baada ya afisi ya mkuu wa mashtaka ya umma kuwasilisha ombi katika mahakama kuu la kufutiliwa mbali dhamana iliyopewa wasichana hao.

Wakati huo huo, jaji Chepkwonyi amemwagiza msimamizi mkuu wa gereza la Shimo La Tewa Samuel Karanja Nyutu kufika mahakani kujibu mashtaka ya kukiuka agizo la mahakama kwa kukataa kuwaachilia washtakiwa hao licha ya mahakama kuwatoza dhamana ya shilingi laki tano kila mmoja.

Hatua hii inajiri baada ya mawakili wa washukiwa hao, wakiongozwa na wakili Hamisi Mwadzogo, kuwasilisha ombi katika mahakama kuu la kutaka kuchukuliwa hatua za kisheria kwa afisa huyo kwa kukiuka agizo la mahakama.

Wanne hao Ummulkheir Abdullah kutoka Zanzibar mwenye umri wa miaka 21, Mariam Said Aboud pamoja na Khadija Abubakar wenye umri wa miaka 19 wote kutoka Malindi wanadaiwa kuwa wanafunzi walioahidiwa ufadhili wa kimasomo, huku Halima Aden akikamatwa katika Kaunti ya Machakos kwa tuhuma za ugaidi.