Shirika la Residents Land Protection Organisation of Kenya limeunga mkono uamuzi wa mahakama ya juu kuhusu mvutano baina ya Wizara ya Ardhi na Tume ya kitaifa ya ardhi nchini NLC.
Mwenyekiti wa shirika hilo, Dewelly Nyambu, alisema kwamba hatua hiyo inalenga kuwaunganisha Wakenya na kusitisha malumbano ya kila uchao baina ya sekta hizo mbili ili kuona kwamba mwananchi anapata haki yake ya ardhi kikamilifu.
Akizungmza na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumanne, Nyambu alisema kwamba cha msingi ni kuona kuwa tume hiyo inakagua vyema ardhi za wananchi zilizo na mvutano, na kulitatua swala hilo bila ya kuegemea upande wowote, kabla ya Wizara ya ardhi kutoa hati miliki za ardhi ili kuzuia mizozo ya ardhi nchini.
"Tunaipongeza mahakama jinsi ilivyotatua mzozo wa mamlaka baina ya wizara ya ardhi na tume ya kitaifa ya ardhi, lakini tungetaka kuona tume hiyo ikifanya ukaguzi wa kina katika ardhi za Pwani ili wizara ya ardhi ikitoa hati miliki swala la unyakuzi wa ardhi liwe limetatuliwa,” alisema Nyambu.
Kauli ya Mwenyekiti huyo inajiri huku wananchi hususan wa eneo la Pwani, wakiitaka serikali kutatua mizozo ya ardhi sambamba na kusitsisha unyakuzi wa ardhi unaondelezwa na baadhi ya mabwenyenye na kuwaacha wenyeji wakiangaika.