Viongozi wa kanisa wanaopanga kuandaa ibada za usiku wakati huu wa sherehe za Krismasi na mwaka mpya sasa watalazimika kuarifu idara ya usalama kabla kufanya hivyo ili kupewa ulinzi.
Akizungumza katika mkutano na viongozi wa kanisa eneo la Kisauni siku ya Jumanne, naibu kamishna wa kaunti ya Mombasa Julius Kavita alisema idara ya usalama itahitaji kujua ni kanisa lipi na ni eneo gani linahitaji maafisa wa usalama.
''Kama viongozi wa kanisa lazima mshirikiane nasi ili tuhakikishe kuwa hali ya usalama ya waumini wenu ipo sawa mnapofanya ibada za usiku,'' alisema Kavita.
Kavita pia alihimiza makanisa kuweka taa za usalama na kuhakikisha kuwa waumini wote wanakaguliwa kabla kuruhusiwa kuingia kanisani.
''Sauti za muziki na kipaza sauti pia zisiwe juu kimo cha kunyima wengine usingizi majumbani mwao,'' aliongeza Kavita.
Kwa upande wake OCPD wa Kisauni Richard Ngatia, aliwataka wananchi kuripoti visa vyovyote visivyo vya kawaida katika maeneo yao na kuwa wasiogope kutoa ushahidi mahakamani iwapo watahitajika kufanya hivyo.