Kufuatia ajali ya gari iliyofanyika siku ya Jumapilii katika daraja la Nyali katika barabara kuu ya Mombasa-Mtwapa, Kamishna wa Kaunti ya Mombasa sasa ameamuru kutiwa mbaroni kwa dereva aliyesababisha ajali hiyo na kufunguliwa mashtaka.
Akiongea na waandishi wa habari katika ofisi yake siku ya Jumatatu, Marwa alisema kuwa dereva huyo anafaa kuchukuliwa hatua kali kwa kosa hilo, huku ikiaminika kuwa alikuwa mlevi wakati wa ajli hiyo.
Marwa alisema kuwa imekuwa mazoea miongoni mwa madereva wengi pamoja na watumizi wengine wa barabara kufanya maovu na kuvunja sheria za trafiki na kuepuka mkono wa sheria kwa kutumia njia za mkato.
Kamishna huyo pia aliwaonya madereva ambao wamezoea ya kuendesha magari wakiwa walevi kuwa sheria itawaandama, na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao na kuongeza kuwa idara mbali mbali za kiusalama zitazidi kuweka juhudi na sheria ya nchi hasa ile ya kudhibiti idara ya trafiki inafuatwa ipasavyo.
Ajali hiyo ambayo ilishuhudia majeruhi watatu ilikuwa inaendeshwa kwa kasi ya juu ambapo ilipoteza mwelekeo na kuingia baharini.
Onyo la kamishna Marwa linakuja wakati ambapo kumeshuhudiwa ukiukaji mkubwa wa sheria za trafiki katika Kaunti ya Mombasa, na itakuwa mojawapo ya hatua za kuhakikisha kuwa abiria pamoja na watumizi wa barabara wako salama katika mwezi huu wa sherehe za krismasi.