Mshirikishi mkuu wa usalama katika ukanda wa Pwani Nelson Marwa ameitaka idara ya usalama katika enoo hilo kuwachukulia hatua walinzi wa Gavana wa Mombasa Hassan Joho, Gavana wa Kaunti ya Kilifi Amason Kingi na mwakilishi wa wanawake kaunti ya Kilifi Aisha Jumwa.
Marwa alidai kuwa walinzi hao walitishia usalama wa wananchi katika uchaguzi mdogo wa eneo bunge la Malindi uliofanyika siku ya Jumatatu, kwa kuwashurutisha baadhi ya wakaazi waliofika katika vituo vya kupigia kura kumpigia kura mgombea ambaye hawakusudia.
“Tayari nimepata habari kuwa walinzi wa viongozi fulani walitishia usalama wa wananchi. Nawambia lazima watachukuliwa hatua za kisheria,” alisema Marwa.
Kwenye kikao na waandishi wa Habari mjini Mombasa siku ya Jumatano, Marwa alisema kuwa atahakikisha kuwa walinzi hao wametiwa nguvuni ili waeleze aliyewatuma kuvuruga amani katika uchaguzi huo.
Kufikia sasa, bado Gavana Joho na mwenzake Kingi, pamoja na mwakilishi wa wanawake wa Kaunti ya Kilifi Aisha Jumwa, hawajajibu madai ya Marwa.