Idara ya usalama Kaunti ya Mombasa imewahakikishia wageni wanaopanga kuzuru mjini Mombasa usalama dhabiti, na kuwataka kuondoa hofu ya kuwepo kwa misukosuko ya ukosefu wa usalama.
Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Nelson Marwa amesema kwamba kaunti hiyo iko salama kwani wakazi na maafisa wa usalama wanashirikiana kwa karibu mno kudumisha amani.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Marwa amewataka wageni kutoka mataifa mbalimbali ya magharibi na barani Afrika pamoja na watalii wa nyumbani kujitokeza kwa wingi na kuzuru kaunti hiyo kujivinjari, hasa msimu huu wa shamra shamra za sherehe za krismas na mwaka mpya.
Marwa amesema kwamba kuwasili kwa meli za kitalii zaidi ya nne katika kipindi cha miezi miwili ni ishara kamili kwamba usalama umeimarishwa kuanzia katika Baharini Hindi, huku akisema kwamba maafisa wa usalama wametumwa nyanjani kushika doria kikamilifu.
"Tunawaomba wageni wote wanaonuia kuzuru Mombasa kujivinjari kuondoa hofu na kuja kwa wingi, usalama umeimarishwa kila mahali, maafisa wa usalama wanashika doria," alisema Marwa.
Kwa upande wake meneja mkuu wa shughuli za bandari ya Mombasa Twalib Khamis, halmashauri ya bandari ya Mombasa inapanga mikakati ya kukarabati eneo la kupokelewa watalii wanapowasili katika bandari ya Mombasa litakalogharimu zaidi ya shilingi milioni 100 ili kuimarisha sekta ya utalii nchini.
"Tumetenga zaidi ya shilingi milioni 100 kukarabati jimbo la kupokea watalii wanazuru Mombasa kupitia bandari yetu ya Mombasa kama njia mojawapo ya kuimarisha sekta ya utalii hapa pwani na taifa letu kwa jumla," alisema Khamis.
Hata hivyo, sekta ya utalii inatarajiwa kuimarika zaidi kufuatia kuwasili kwa meli nne za watalii kwa kipindi cha miezi miwili iliyopita, huku bodi ya utalii nchini ikisema kwamba meli zingine mbili za watalii zinatarajiwa kuwasili mwaka huu.