Sasa imebainika kuwa kuna baadhi ya watu wanaotumia ujanja kunufaika kutokana na watoto wanaozurura mitaani maarufu kama chokoraa katika Kaunti ya Mombasa.
Hii ni baada ya watoto hao kueleza kuwa watu tofauti wamekuwa wakiwatembelea na kuwaahidi kuwasaidia, lakini baada ya kuwapiga picha wanatoweka.
Mmoja wa watoto hao, Zakary Mutembei aliambia mwandishi huyu siku ya Jumatatu kuwa watu hao wamekuwa wakiuza picha hizo katika mashirika ya ng’ambo badala ya kuwasaidia.
“Sisi tumejua ujanja wao, wanatuma picha hizo kwa mashirika ya nje na kuchukua fursa hiyo kuomba ufadhili lakini pesa hizo zinapotumwa hatuzifaidi,” alisema kijana huyo.
Aidha, watoto hao wanasema kuwa hawatakubali msaada wa aina yoyote kutoka kwa mtu wasiyemjua, na kutishia kumkabili mtu yeyote wanayemshuku kuwa tapeli.
Kwa upande wake waziri wa vijana kaunti hiyo Mohamed Abas alikiri kuwepo kwa matapeli wanaotumia fursa ya watoto hao kujinufaisha, lakini akaahidi kuwa serikali ya kaunti imeweka mikakati kuwanusuru.
Mombasa ni moja kati ya miji yenye idadi kubwa ya watoto wanaozurura mitaani nchini Kenya, na mashirika mbalimbali yamekuwa yakijitokeza kujaribu kuwanusuru.