Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Waziri wa Elimu nchini Fred Matiang'i amepongezwa kwa kuanzisha ujenzi wa chuo cha anuwai katika eneo la Riragia, eneo bunge la Kitutu Chache Kaskazini.

Hii ni baada ya waziri huyo kuanzisha ujenzi huo siku ya Alhamisi baada ya pendekezo kutoka kwa wakazi na mbuge wa eneo hilo Jimmy Angwenyi.

Wakazi wa eneo hilo walisema kuwa chuo hicho kitakuwa kinatoa usaidizi mkubwa haswa kwa wanafunzi wanaosomea taasisi za kiufundi, ili kujisaidia kwa siku zijazo.

Wakizungumza na mwandishi huyu siku ya Ijumaa katika eneo la Riragia, wakazi wa eneo hlio wakiongozwa na mzee wa kijiji cha Riobiri Peterson Mokua, walimpongeza Matiang'i kwa kuanzisha ujenzi wa chuo hicho.

Kulingana na wakazi hao, wanafunzi wanaotaka kusomea taasisi za kiufundi walikuwa wanalazimika kupata masomo hayo kwingineko.

“Tunasema asante kwa Matiang'i kwa kuendelea kupigania jamii ya Kisii kielimu, ili tuweze kuonekana na kung’ara katika taifa la Kenya,” alisema Mokua.

Aidha, Mbunge wa eneo bunge hilo la Kitutu Chache kaskazini Jimmy Angwenyi na mwenzake wa Kitutu Chache kusini Richard Onyonka walimpongeza waziri huyo kwa kuinua viwango vya elimu kote nchini.