Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Chama cha mawakakili katika kaunti ya Kisii kimetishia kuelekea mahakamani kujua kwa nini wanafunzi 320 katika kaunti hiyo hawakupata matokeo yao ya mitihani yaliyotangazwa wiki jana.

Mawakili hao wakiongozwa na Ocharo Kebiro na Yobesh Onchiri wanataka kujua kwa nini kila wakati baadhi ya wanafunzi katika kaunti ya Kisii matokeo yao ya mitihani hufutuliwa mbali.

Wakizungumza siku ya Jumapili mjini Kisii, mawakili hao walisema tayari wameanzisha uchungunzi kubaini kiini kilichosababisha matokeo ya wanafunzi hao kufutiliwa mbali kisha waelekee mahakamani ili matokeo ya wanafunzi hao yaachiliwe.

“Kila mwaka kaunti ya Kisii lazima idaiwe kuhusika katika visa vya udanganyifu, wakati huu tutaenda mahakamani ili kila mwanafunzi apate matokeo yake ya mitihani,” alisema Ocharo.

“Tunahitaji watoto wetu kuendelea mbele kielimu bila kuzuiliwa kwa kudaiwa kuibia mtihani kila wakati, lazima haki itendeke kwa kila mmoja,” alisema Onchiri.

Kwa upande wa mkurugenzi wa elimu katika kaunti ya Kisii Richard Chebkawai alisema wanafunzi 320 ambao walikosa majibu ya mitihani yao wanatoka katika wilaya za Masaba kaskazini, Kisii ya kati, Gucha, Kenyenya, Gucha kusini na Marani ambao walidaiwa kupatikana na simu za mkononi na vijikaratasi vya kuibia.