Share news tips with us here at Hivisasa

Vijina na wanawake katika eneo la Pwani wamehimizwa kujitokeza kwa wingi na kujisajilia kama wapiga kura na kushiriki vyema katika uchaguzi mkuu ujao, ili kuwabandua mamlakani viongozi wasiowajibika.

Kulingana na Mwakilishi wa Wanawake katika Kaunti ya Mombasa Mishi Mboko, viongozi wengi waliochaguliwa wameshindwa kuwatekelezea wananchi masuala muhimu mashinani, hivyo basi wakati umefika wakuwaondoa mamlakani.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Alhamisi katika mkutano wa wanawake, Mboko alisema kuwa iwapo vijana na akina mama watajitokeza kwa wingi, basi uongozi wa taifa hili utabadilika kwani viongozi walio mamlakani wamezongwa na kashfa za ufisadi.

“Tafadhalini akina mama wakati umefika sasa kujitokeza kwa wingi na kubadili uongozi wa taifa hili kwa kujisajili kama wapiga kura na kushiriki moja kwa moja katika uchaguzi, ili kuwaondoa wale viongozi wanyanyasaji,” alisema Mboko.

Wakati uo huo, Mboko aliwasuta viongozi waliokihama chama cha ODM kwa kusema kuwa ni viongozi wenye tamaa ya uongozi, na wasiojali maslahi ya wakazi.

“Kuna viongozi wengine waliohama chama chetu kwa tama ya uongozi wakidhani kule wameenda watafaidi. Sisi tunawaambia wabaki huko walikokwenda kwani wakifukuzwa sisi hatutawaruhusu kwa chama,” alisema Mboko.

Kauli ya Mboko inajiri huku Tume huru ya uchaguzi na uchaguzi na mipaka IEBC ikiazimia kusajili wapiga kura elfu nne katika zoezi linaloendelea kote nchini.