Gavana wa Kaunti ya Nakuru Kinuthia Mbugua ameitaka serikali kuu kuongeza mgao wa fedha za basari.
Mbugua alisema kuwa huenda mamia ya wanafunzi waliomaliza darasa la nane wakakosa nafasi za kujiunga na shule za upili kutokana na karo za juu zinazotozwa.
Akizungumza mjini Naivasha siku ya Ijumaa baada ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo, Mbugua alisema kuwa wazazi wengi hawawezi kulipa karo hizo.
Alitoa changamoto kwa serikali kuu kuingilia kati ili kuokoa wanafunzi hao, kwa kuongeza mgao wa fedha za basari, na kushinikiza kutekelezwa kwa sera za elimu kuhusu kiwango cha karo.
Huku akikaribisha msimamo wa Wizara ya Elimu kuhusu kutoongeza karo za shule, gavana huyo alisema kuwa huenda agizo hilo lisitekelezwe inavyofaa.
"ikiwa agizo hilo halitazingatiwa, huenda usalama wa kitaifa ukaadhirika kwa sababu baadhi ya vijana huenda wakajiunga na vikosi vya uhalifu na kigaidi, baada ya kukosa nafasi ya kuendelea na masomo,” alisema Mbugua.
Hata hivyo, Gavana Mbugua alisema kuwa wadi zote 55 za kaunti ya Nakuru zimepokea shilingi milioni mbili za basari, kusomesha wanafunzi waliofanya vyema kutoka familia maskini.