Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mbunge wa Kitutu Masaba Timothy Bosire ameahidi kufadhili masomo ya wanafunzi waliofaulu katika mtihani wa KCPE, wanaotoka katika familia maskini.

Bosire alisema kuwa masomo ya wanafunzi hao yatafadhiliwa na pesa za hazina ya ustawishaji wa maeneo bunge CDF.

Akihutubu katika eneo la Kemera siku ya Jumapili, Bosire alisema kuwa afisi yake itawafadhili wanafunzi hao huku akiwahimiza wazazi kuwasilisha majina na alama za wanafunzi hao kwa afisi yake punde tu uteuzi wa kujiunga na shule za upili utakapo tamatika.

Bosire alisema kuwa pia atawasaidia wanafunzi maskini watakao jiunga na shule za kaunti.

"Ninajua kuwa kupata nafasi kwenye shule za upili za kitaifa sio jambo rahisi. Wanafunzi waliofanya vizuri na kupata alama ambazo zitawawezesha kujiunga na shule hizo watafadhiliwa kusoma na afisi yangu kupitia kwa hazina ya CDF,” alisema Bosire.

Aliongeza, “Hilo halimaanishi kwamba sitawasaidia wanafunzi wengine maskini kwa kuwa nitahakikisha kuwa hata wao pia wameshughulikiwa."

Bosire aidha alisema kwamba kamati ya hazina ya CDF itasitisha ufadhili wa masomo kwa wanafunzi ambao hawataonyesha matokeo bora katika mtihani yao kila mwisho wa muhula.

Alisema kuwa kamati hiyo pia itafadhili watu watakao wapa motisha wanafunzi shuleni kutia bidii masomoni kwa njia yakuwaongelesha.

"Wanafunzi watakaonufaika na mpango huu shatri wawe na matokeo bora kila mwisho wa muhula. Pia nitafadhali washauri watakao wahamasisha wanafunzi kutia bidii masomoni,” alisema Bosire.