Share news tips with us here at Hivisasa

Baadhi ya wabunge wa Mrengo wa Cord katika eneo la Pwani wameahidi kuwasilisha mswada bungeni wa kushinikiza serikali kuitengea Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini (IEBC) fedha zaidi ili kufanikisha zoezi la usajili wa wapiga kura nchini.

Akiongea mjini Mombasa siku ya Jumatano, Mbunge wa Mvita, Sharrif Nassir alisema kuwa ipo haja ya serikali kuiongezea fedha tume hiyo, na kudai kuwa jinsi serikali ilivyopinga pendekezo la IEBC, imeonyesha wazi kuwa kuna njama potovu.

Nassir aliahidi kuhakikisha kuwa tume hiyo inaangaziwa vyema ili kuona kwamba uchugazi mkuu wa mwaka wa 2017 ni wa huru na haki ili kuhakikisha kuwa uchaguzi huo haukumbwi na udanganyifu.

"Kama Cord tumejiandaa kikamilifu kuwasilisha mswada mbunge utakaoishinikiza serikali kuiongezea fedha tume hiyo na kufanikisha uchaguzi mkuu wa huru na haki na kuzuia udanganyifu,” alisema Nassir.

Mbunge huyo wa Mvita amewataka wakaazi kujitokeza kwa wingi na kujisajili kama wapiga kura ili kushiriki vyema katika uchaguzi mkuu ujao, na kuwachagua viongozi waadilifu wataoleta mwamko mpya nchini.