Share news tips with us here at Hivisasa

Mbunge wa eneo bunge la Kibra Bwana Ken Okoth ameilaumu serikali kuu kwa kusema kuwa imezembea katika shuguli ya ujenzi wa shule za umma katika mtaa wa Kibera.

Ken Okoth, ambaye pia ni mwanachama wa kamati ya bunge kuhusu elimu alisema kuwa suala hilo limesababisha kuongezeka kwa idadi ya shule zisizo rasmi katika mtaa wa Kibera.

Akizungumza afisini mwake siku ya Jumamosi, Okoth alisema kuwa wazazi kwenye mtaa wa Kibera wamelazimika kukimbilia shule hizo ambazo ni za kibinafsi, kwa kuamini zinatoza karo ya kiwango cha chini ili angalau kuwapa wanao haki msingi ya elimu.

“Ukweli wa mambo ni kwamba ni jukumu la serikali kuhakikisha kuna walimu wa kutosha, madarasa ya kutosha na shule za kutosha ili kuhakikisha kwamba watoto wanapata elimu ya kutosha, ya haki na ya bure. Mtaa wa Kibera una shule tisa pekee za msingi ilhali idadi ya watoto ni kubwa, hali inayowalazimu wazazi kutafuta mbinu mbadala za kuwaelimisha watoto wao,” alisema Okoth.

Mbunge huyo aliwahimiza wadau wenye nia njema kuendelea kujenga shule hizo ili kuwawezesha watoto kupata elimu kwa manufaa yao ya baadaye.

“Tunawaomba wadau ambao wamefungua shule za kibinafsi katika mtaa wa Kibera kujaribu kuhakikisha kuwa shule hizo ni nzuri kwani wazazi wanakimbilia shule hizo kufuatia uchache wa shule za umma,” alisema Okoth.

Aidha, aliongeza kuwa madarasa ya shule za msingi katika mtaa wa Kibera yataboreshwa na pia idadi ya shule za upili kuongezwa.

Baadhi ya wadau katika sekta ya elimu ikiwemo Miungano ya walimu ya Knut na Kuppet imetilia shaka kiwango cha elimu kinachotolewa na shule za kibinafsi, wakihoji kwamba walimu wanaoajiriwa kuwafunza wanafunzi kwenye shule hizo hawajahitimu, na kwamba mtaala unaotumika kutoa masomo haujaidhinishwa na taasisi inayosimamia mtaala nchini KICD.