Mbunge wa eneo bunge la Kitutu Masaba kaunti ya Nyamira Timothy Bosire ameombwa kujenga vyoo vya shule ya msingi ya Riamogaka katika eneo bunge hilo baada ya vyoo hivyo kuanguka juma lililopita na kupelekea maafisa wa afya kufunga shule hiyo.
Wakizungumza na waandishi wa habari siku ya Alhamisi katika eneo hilo la Riamogaka, wazazi wa shule hiyo wakiongozwa na Patrick Omae na Shadrack Mogaka waliomba mbunge wao kusaidia shule hiyo kujenga vyoo hivyo ili wanafunzi warudi shule.
“Wiki jana wanafunzi walitumwa nyumbani baada ya vyoo vya shule kuanguka nao maafisa wa afya waliagiza shule kufungwa hadi vyoo vipya vijengwe, tunaomba mbunge wetu Timothy Bosire asaidie shule hii kwa ujenzi wa vyoo hivyo,” alisema Omae.
Wakati huo huo, wazazi hao pia waliomba wahisani wengine wema kujitokeza kutoa usaidizi kwa shule hiyo ili wanafunzi kurejelea masomo yao kama kawaida.
“Tunaomba wahisani wema kujitokeza ili kushirikiana na serikali kupitia mbunge wetu Bosire ili vyoo vipya vijengwe katika shule hii,” alisema Mogaka.