Mbunge wa eneo bunge la Kitutu Masaba Timothy Bosire amejitokeza kumtaka kinara wa walio wengi kwenye bunge la kitaifa Aden Duale kujiuzulu kutoka kwa wadhifa wake ili kuruhusu uchunguzi kufanywa dhidi yake.
Akihutubia kikao cha wanahabari siku ya Jumatano, Bosire alisema kuwa wakati umefika kwa kinara huyo wa Jubilee kwenye bunge la kitaifa kujiuzulu mara moja ili kuruhusu uchunguzi kufanyika dhidi yake.
"Duale amekuwa akiwatusi viongozi mbalimbali wa kisiasa wanapohusishwa na madai ya ufisadi, na kwa kuwa sasa ni bayana kwamba aliyekuwa waziri wa ugatuzi Anne Waiguru alimtaka kwenye haki ya kiapo kuwa yeye ni miongoni mwa watuhumiwa yafaa ajiuzulu mara moja," alisema Bosire.
Bosire aidha alisema kuwa iwapo Duale atajiuzulu, vita dhidi ya ufisadi nchini vitaonekana kuwa na makali kwa kuwa kiongozi huyo amekuwa akishurutisha viongozi wengine kujiuzulu pindi wanapohusishwa na madai ya ufisadi.
"Nafikiri Duale anafaa kujiuzulu iwapo kwa kweli yeye ni miongoni mwa viongozi wanaounga mkono vita dhidi ya ufisadi kwa maana hili ni tatizo sugu la uvujaji wa millioni 700, pesa zilizopotea kwa njia isiyoeleweka, na ndio maana sharti ajiuzulu ili isiwe kwamba yeye ni kuwataka viongozi wengine kujiuzulu," aliongezea Bosire.
Bosire vilevile aliyashtumu mashirika ya kufanya upelelezi nchini kwa kushindwa kumchukulia hatua Aden Duale baada yake kukataa kuwataja watu anaowajua kuhusika na ufadhili wa kundi la kigaidi la Alshabaab miezi kadhaa iliyopita.
"Idara ya ujasusi nchini ilishindwa kabisa kumchunguza Duale wakati aliposema kuwa anajua watu wanaofadhili kundi la kigaidi la Alshabaab na hadi sasa hamna hatua iliyochukuliwa dhidi yake na sharti aondoke ofisini ili achunguzwe iwapo anahusika kwenye sakata ya NYS," alihoji Bosire.