Meli ya kitalii ya Ms Silver Cloud imetia nanga katika Bandari ya Mombasa ikiwa na abiria 197 kutoka nchini Zanzibar.
Kulingana na mkurugenzi mkuu wa Chama cha Watalii nchini 'Kenya Coast Tourist Association’ Mohammed Hersi, kuzuru kwa meli za kitalii katika Bandari ya Mombasa kumeanza kuimarisha sekta ya utalii ambayo ilikuwa ikikumbwa na changamoto.
Akiongea na wanahabari baada ya kuwapokea watalii hao katika bandari ya Mombasa siku ya Jumanne, Hersi alisema kuwa baadhi ya watalii watasalia eneo hilo huku wengine 232 wakiabiri meli hiyo kuelekea nchini Dubai mwendo wa saa moja jioni.
Hersi alisema kuwa Waziri wa Utalii nchini Najib Balala pamoja na Mkurugenzi mkuu wa Bodi ya Utalii nchini Muriithi Ndegwa wameelekea nchini Uingereza kuuza taifa hili katika maswala ya kitalii na kuwavutia wageni wengi kuzuru nchini.
"Tunafurahi sana kupokea wageni kutoka mataifa mbalimbali kuja Mombasa kutalii. Hatua hii itaimarisha sekta ya utalii kwani meli hii ni meli ya nane kutia nanga Mombasa, tangu kuwepo na changamoto za kiusalama. Tupo na matumaini kuwa sekta hii itaimarika zaidi,” alisema Hersi.
Katibu wa bodi hiyo Allan Njoroge alipongeza kuongezeka kwa meli za kitalii nchini, huku akiitaka serikali kuzidisha juhudi zake za kuimarisha usalama wa majini na angani, ili kuondoa hofu kwa baadhi ya mataifa ya magharibu na kuruhusu raia wao kuzuru Kenya.
Meli hiyo imewasili na watalii 61 kutoka Marekani, 42 kutoka Uingereza, wasita kutoka Russia, wasaba kutoka Sweden na watatu kutoka Afrika Kusini, ambao wanatarajiwa kuzuru maeneo mbalimbali ya kitalii ikiwemo mbuga za wanyama pori.