Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Meneja wa Kampuni ya sukari ya Ramisi iliyoko Kaunti ya Kwale ametozwa dhamana ya Sh100,000 kwa madai ya kuajiri raia kutoka India bila kibali cha kufanya kazi humu nchini.

Siku ya Alhamisi, mahakama ilielezwa kuwa kati ya Septemba 24 na Oktoba 27, 2015, Patrick Chebosi, anadaiwa kumuajiri Mahetre Bopu Dattatrya ambaye ni raia wa India, kinyume cha sheria kufanya kazi ya ufundi katika kampuni hiyo.

Aidha, meneja huyo na wafanyikazi wengine wanane wamekabiliwa na shtaka la kukataa kuwakabidhi maafisa kutoka afisi ya uhamiaji vyeti vya kusafiria na kuzaliwa vya wafanyikazi kutoka nchi ya India.

Patrick Chebosi na wenzake walikanusha mashtaka yote.

Akitoa dhamana hiyo, siku ya Ijumaa, Hakimu Mkuu wa Mombasa Diana Mochache alisema kuwa kila mshtakiwa yuko na haki ya kupewa dhamana kwa mujibu wa katiba ya nchi na kuwataka washtakiwa hao kutokosa vikao vya kesi yao.

Kesi yao itatajwa Novemba 3, 2015.