Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Serikali ya kitaifa imeahidi kutatua suala tata la ardhi sawia na dhulma za kihistoria katika kanda ya Pwani.

Waziri wa Ardhi Profesa Jacob Kaimenyi alisema siku ya Jumatatu kuwa serikali inafahamu changamoto wanazopitia Wapwani, lakini kupitia kuundwa kwa tume ya kitaifa ya ardhi, suala la ardhi litasuluhishwa.

Akiongea huko Watamu kwenye warsha iliyoshirikisha bodi za ardhi za kaunti zote eneo la Pwani pamoja na washikadau wengine, Kaimenyi alisema ni kinyume cha sheria kwa mtu yeyote kuvamia ardhi za wengine, akisema serikali itawashirikisha washikadau wote katika juhudi za kutatua matatizo ya ardhi.

Naye mwenyekiti wa tume ya kitaifa ya ardhi Mohamed Swazuri alisema anayo matumaini ya kutatuliwa kwa masuala tata ya ardhi kufuatia kuundwa kwa bodi za ardhi za kaunti.

Swazuri alisema hakuna madhara yoyote kwa ardhi za Pwani kuwa chini ya usimamizi wa serikali, ambapo asilimia 70 ya ardhi za Pwani zimeorodheshwa kuwa chini ya serikali ya kitaifa.

Haya yanajiri siku moja baada ya mwanamume mmoja kuawa katika mzozo wa shamba eneo la Kikambala.