Mjane mwenye umri wa miaka 65 mjini Nakuru anapanga kuzika mgomba wa ndizi baada ya hospitali moja ya kibinafsi kumkataza mwili wa mwanawe aliposhindwa kulipa milioni kumi na saba.
Bi Mary Nyageiro anasema kuwa jamaa na marafiki wake waliokuwa wakikutana nyumbani kwake katika mtaa duni wa Mwariki kuchanga pesa waliacha kuhudhuria mikutano hiyo.
Bi Nyageiro anasema kuwa, licha ya kumpoteza mwanawe, Freddy Nyageiro, ambaye alikuwa akitegemewa na familia kwa mahitaji yote, sasa hawezi kumzika kwa sababu hospitali imekataa na mwili wake hadi atakapolipa deni hiyo.
“Nimepanga kuzika mgomba wa ndizi ambao utakuwa ishara ya mwili huo kwa sababu sina uwezo wa kulipa pesa hizo,” alisema Bi Nyageiro.
Anasema kuwa mwanawe, ambaye alikuwa na umri wa miaka 37, alilazwa katika hospitali ya Karen, Nairobi, akiugua maumivu tumboni.
Baada ya wiki moja, daktari aliyekuwa anamtibu alisema alikuwa na tatizo la kongosho na kuwa alihitaji kufanyiwa upasuaji wa dharura.
“Baada ya upasuaji, hali yake iliendelea kudhoofika na tukaingiwa na wasiwasi. Tuliomba wasimamizi wa hospitali hiyo waturuhusu kumhamishia hospitali nyingine lakini walikataa wakisema ingekuwa vigumu kumbeba kwa sababu ya hali yake,” alieleza Bi Nyageiro.
Baada ya miezi miwili, mwanawe alifariki na bili ya matibabu yake ilikuwa imefikia mamilioni ya pesa.
Bi Nyageiro alijaribu kuchangisha pesa kutoka kwa jamaa na marafiki ili kulipa deni hiyo lakini hazikutosha.
“Nilipata shilingi milioni moja pekee na nikalipa hospitalini,” aliongeza Nyageiro.
Msemaji wa hospitali ya Karen, alisema familia ya marehemu inatakiwa kupeleka ombi rasmi ili wapewe mwili na pia kutoa hakikisho kwamba watalipa pesa kwa muda watakaokubaliana.
“Ombi lao litawasilishwa kwa kamati simamizi ya hospitali ili kujadiliwa kabla ya kupewa mwili,” alisema msemaji huyo.